Vyombo vya habari vya Syria Jumatano asubuhi vilitangaza kuwa suati za milipuko mikubwa zimesikika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus. Tovut ya gazeti la al Watan pia imeandika kuwa, utawala wa Israel umeshambulia eneo la al Kiswah, kusini magharibi mwa Damascus. Aidha ndege zisizo na rubani za Israel ziliruka katika anga ya mikoa ya Quneitra na Dara'a, na kisha ndege za kivita za utawala huo zilishambulia eneo la "Tal al-Harah" katika mkoa wa Dara'a.
Sambana na mashambulizi hayo, televisheni ya al Mayadeen ilitangaza kuwa wanajeshi wa utawala huo ghasibu wameingia katika kijiji cha Ain al-Bayda kilichoko kaskazini mwa mkoa wa Quneitra. Wanajeshi vamizi wa Israel pia walivamia kijiji cha Saida huko Golan kati ya mikoa ya Dara'a na Quneitra na kuvuka maeneo hayo. Sambamba na mashambulizi makali ya anga dhidi ya Damascus na kusini mwa Syria, vifaru vya utawala huo vimewekwa katika ukanda wa mpaka wa majimbo ya Dara'a na Quneitra, na wanajeshi wa Israel wameingia katika baadhi ya vijiji.
Jeshi la Israel limethibitisha mashambulizi yake hayo na kudai kuwa lililenga shabaha za kijeshi kusini mwa Syria, yakiwemo makao makuu na maeneo mengine ikiwa ni pamoja na zana za kijeshi.
Israel ilikuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya Syria wakati wa utawala wa Bashar al Assad, rais wa zamani wa nchi hiyo. Pamoja na hayo, baada ya kuondolewa madarakani Bashar al Assad, mashambulizi dhidi ya nchi hiyo yanatekelezwa kwa urahisi kabisa na bila ya majibu. Kwa upande mmoja, utawala wa Kizayuni unaamini kuwa, hakuna serikali thabiti na yenye nguvu huko Syria, na kwa upande mwingine, watawala wapya wa Syria hadi sasa hawajatoa jibu na radiamali yoyote kali dhidi ya mashambulizi ya Wazayuni.Utawala wa Kizayuni wa Israel umeharibu na kusambaratisha nguvu na uwezo wote wa kijeshi wa Syria kwa kutekeleza mashambulizi ya siku kadhaa nchini humo baada ya kuanguka serikali ya Assad.
Swali linaloulizwa hapa ni kuwa, Israel unakusudia nini kwa kufanya mashambulizi mtawalia dhidi ya maeneo mbalimbali ya Syria?
Inaonekana kuwa lengo kuu la utawala wa Kizayuni ni kuikalia kwa mabavu ardhi ya nchi ya Syria. Utawala huo ambao baada ya kuanguka serikali ya Assad ulikalia kwa mabavu sehemu ya maeneo ya kijiografia ya Syria, unakusudia kuyaunganisha maeneo hayo na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Kwa kufanya mashambulizi mara kwa mara dhidi ya Syria, Israel inajaribu kuibua hofu na ukosefu wa amani miongoni mwa wakazi wa maeneo yanayokabiliwa kwa mabavu ili raia hao walazimike kuyahama makazi yao. Kufuatia harakati hizo baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wamelazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia mikoa ya kaskazini mwa Syria.
Lengo jingine la utawala wa Kizayuni ni kwamba sambamba na Israel kuzuia serikali mpya ya Syria kuanzisha kambi ya kijeshi kuisni mwa nchi hiyo, utawala huo wenyewe unataka kuanzishe kambi ya kijeshi katika eneo la kijiografia la Syria.
Israel Katz Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametishia kuwa watawala wapya wa Syria hawataruhusiwa kuanzisha kambi za kijeshi kusini mwa nchi hiyo, na kudai kuwa Tel Aviv haitaruhusu eneo la kusini mwa Syria liwe kama kusini mwa Lebanon.
Tovuti ya Ynet ya gazeti la Yedioth Ahronoth pia imeripoti kuwa utawala ghasibu wa Israel umeingia katika awamu ya utekelezaji wa mpango wake wa kuingia na kuyakalia kwa mabavu maeneo ya kusini mwa Syria. Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari vya Kiibrania, Tel Aviv inapanga kulikalia kwa mabavu eneo lenye ukubwa wa kilomita 15 ndani ya ardhi ya Syria, na wakati huo huo, kudhibiti masuala ya kiitelijinsia kusini mwa Syria kwa kuanzisha "eneo la ushawishi" la kilomita 60 ndani ya ardhi ya nchi hiyo.Ombwe unaoshuhudiwa sasa nchini Syria na hali ya serikali inayotawala nchini humo pia vimeupa utawala huo ghasibu fursa ya kutekeleza malengo yake kirahisi.
342/
